MFUNGO WA SIKU 10 WA KILA MWISHO WA MWEZI | SIKU YA TISA

KANUNI YA MUDA (THE PRINCIPLE OF TIME).

MAMBO UTAKAYOJIFUNZA;

1. Muda ni rasilimali pekee ya kutimiza kusudi na maono yoyote makubwa ULIYONAYO (Mhubiri 3:1).

2. Muda uliopewa umehesabiwa hivyo unahitaji hekima na nidhamu katika matumizi ya kila siku yako moja (Ayubu 14:1-6, Zaburi 90:12).

3. Madhara ya kutumia vibaya muda wa maisha yako

4. Faida za kutumia muda kwa hekima na nidhamu katika kufanikisha maisha ya mtu

5. Mbinu za kutumia ili uwe na matumizi sahihi ya muda

6. Hitimisho: Maneno ya hekima kuhusu muda toka kwa Mwl. D.C.Kabigumila

Karibu na utulie kujifunza tunapopitia point moja moja hapo juu.

1. MUDA NI RASILIMALI PEKEE YA KUKUSAIDIA KUTIMIZA KILA KUSUDI NA MAONO ULIYONAYO

•Kila jambo linalofanyika duniani, jema au baya, la kujenga au la kubomoa, linahitaji MUDA ili kulifanya.

•Watu wanaokaa maabara wakizalisha tiba za magonjwa, au wakifanya majaribio ya teknolojia itakayokuja kuboresha maisha ya wengi, hukaa masaa, wiki, Miezi na hata miaka wakitafuta masuluhisho hayo.

Ndugu Edson Thomas, mtu aliyefanya majaribio ya kubadili UMEME MWENDO (current electricity) kuwa NURU KATIKA TAA (Light bulb), ALIFANYA MAJARIBIO ELFU TISA MIA TISA NA TISINI NA TISA, kabla ya jaribio la ELFU KUMI halijafaulu kupata njia au kanuni ya kugeuza nishati ya umeme kuwa nuru/mwanga!

Ili kufanya jaribio moja alitumia masaa na hata wiki kadhaa. Kwa majaribio 10,000 atakuwa alitumia asilimia kubwa ya maisha yake kufanikisha ugunduzi huu muhimu ulioleta urahisi wa maisha kwa dunia yake, kiasi cha hata sisi ambao hatukumuona tunasoma habari zake na utumiaji sahihi wa muda uliopelekea mpenyo huu mkubwa kwa wanadamu na dunia yake!

Naamini kila mmoja wetu, Mungu amekubebesha majibu na suluhu za watu wengi, wengine mna majibu ya familia zenu, koo zenu, kanda mlizoko, na wengine mna majibu ya taifa letu zuri, na kuna wengine mmeumbwa kuleta mwanga na nuru kwa ajili ya Afrika nzima, na wengine wetu tuna majibu ya dunia nzima.

Kwa maneno mepesi, hakuna hata mmoja wetu ambaye ni bahati mbaya, umezaliwa kwa kusudi ukiwa kazi kamilifu ya Mjenzi mwenye hekima kuu (Mungu)!

Na unapaswa kukamilisha hayo mambo uliyobeba kama mawazo, mipango, malengo, ndoto na maono ndani ya MUDA WAKO WA KUISHI AMBAO HATA HATUJUI UNAISHA LINI MAANA HILO NI FUMBO.

Rasilimali kubwa ULIYONAYO sasa ni muda. Kila mmoja wetu ana masaa 24 ya siku yake moja, yaani masaa 12 ya mchana, na masaa 12 ya usiku.
Namna utakavyoyatumia, ndiyo itakayo amua UTATIMIZA KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO AU UTAKUFA KAMA KUKU, BILA SAUTI, JINA NA HESHIMA!

Maandiko yanasema;
“Kwa KILA JAMBO (Maono, mipango, ndoto, wazo) kuna MAJIRA YAKE na kuna WAKATI MAALUM kwa kila KUSUDI chini ya mbingu (duniani)…”
(Mhubiri 3:1).

Kwa mujibu wa andiko hili tunajifunza yafuatayo;

a) Kila jambo unalotamani kulifanya, linahitaji muda

b) Kila jambo lina wakati wake maalum, ambapo ukikosea huo wakati utabaki unajilaumu au kujuta, na ukipatia wakati sahihi wa kufanya jambo, utaacha alama isiyofutika!

c) JAMBO lililofanyika ndani ya wakati wake linakuwa na mkono wa Mungu wa kulifanya lifanikiwe automatic, na jambo lililokosewa wakati wake linatumia nguvu nyingi mno kulifanya.

d) Kila KUSUDI ambalo Mungu amempatia mtu duniani lina wakati wake wa kulifanyia kazi, UKIUKOSEA HUO WAKATI unaweza kufa bila kulifanya, au ukafanya chini ya kiwango.
Mfano: Mtu ambaye sasa ana miaka 70, na kumbe Mungu alimuumba mwaka 2000 awe Rais wa Tanzania, badala ya yeye kugombea mwaka huo, akasema “NINA KIBALI KWA WATU, WANANIELEWA, NITAGOMBEA 2010, acha Swahiba wangu John agombee kwanza, akimaliza awamu zake nitagombea na mimi na hakuna wa kunizuia nitakuwa Rais tu wa Tanzania”

Nakuhakikishia mtu huyu hatakuwa Rais kamwe. Si kwa sababu hakupaswa kuwa, la hasha! Bali ni kwa sababu HAKUJUA WAKATI WAKE WA KUWA RAIS ULIKUWA UPI.

Ndivyo ilivyo kwangu na kwako, tusipojua kuhusu wakati upi nifanye lipi, na majira gani nifanye nini, TUTAJIKUTA TUMEUNGANA NA WAZEE WETU KULIA KILIO MAARUFU CHA “NINGEJUA” AU “NINGEKUA NARUDI UTOTONI AU UJANANI”..!

Ninakuombea Mungu afungue akili yako, na moyo wako upate kujua mambo sahihi ya kufanya ndani ya majira na muda ulionao hapa duniani, na vipindi mbalimbali vya maisha yako.

Kama Mungu aliwapa wana wa Isakari UWEZO WA KUJUA NYAKATI NA MAJIRA NA MAMBO SAHIHI YA KUFANYA, anaweza kumpatia mtoto wake yeyote atakayemuomba kwa dhati baada ya kuelewa umuhimu wa rasilimali hii muhimu iitwayo MUDA!
(Habari za wana wa Isakari utazipata 1NYAKATI 12:32, nakushauri ujiombee upewe hekima hiyo ili ikusaidie kujua nini cha kufanya kwenye kila hatua na kila ngazi ya maisha yako).

2. MUDA WA MAISHA WA MWANADAMU “UMEHESABIWA” HIVYO ANAHITAJI “HEKIMA NA NIDHAMU” KUWEZA KUACHA ALAMA DUNIANI.

Maandiko:

“Siku za mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke, NI CHACHE TENA ZIMEJAA TABU…Huchanua kama ua, na kisha hunyauka… Nawe (Mungu) UMEMWEKEA MPAKA AMBAO HAWEZI KUUVUKA”
(Ayubu 14:1-5).

Mambo ya kujifunza katika andiko hapo juu;

√ Kila mwanadamu ambaye ana mama, maisha yake yamehesabiwa, yanaanza anapozaliwa na yanaisha siku ya kifo chake.

√ Kwa mujibu wa Mungu, siku za maisha za mtu ni chache hata kama ataishi miaka 100, 90, 80, 70, 60 nakadhalika. Bahati mbaya tunaishi kwenye kizazi cha siku za mwisho ambako VIJANA WENGI WANAKUFA HATA KABLA YA KUFIKIA MIAKA 30, kwa sababu ya dhambi na vita kubwa ya Shetani dhidi ya vijana katika siku za mwisho!

√ Mungu ameshaweka mpaka au ukomo wa maisha ya mtu ambao hakuna awezae kuuvuka au kuukwepa, Mpaka huo unaitwa KIFO.
Hivyo kabla ya maisha ya mtu kufikia ukingoni, anapaswa awe na hekima na nidhamu ya Kimungu, itakayomsaidia kutumia muda wake duniani kwa faida na kuacha alama isiyofutika hata akiwa ameshaondoka duniani!

HEKIMA KATIKA MATUMIZI YA MUDA.

“…UNIFUNDISHE KUZIHESABU SIKU ZANGU, UKANIPATIE MOYO WA HEKIMA…”
(Zaburi 90:12).

•Bila Mungu kukupatia hekima, utaishi maisha ya kupoteza na kuchezea maisha na ukija kushtuka, umefika mwisho na hujaacha alama wala huna mguso kwa dunia yako.

•Mungu asipokupatia moyo wa hekima, utakuwa mtu wa kuahirisha ahirisha mambo ya muhimu, kwa kisingizio cha hata kesho nitafanya, au bado deadline iko mbali.

•Mungu asipokupatia moyo wa hekima, utahesabu miaka mingi ya kuishi na birthday kibao lakini HUNA IMPACT KWA JAMII HATA KIDOGO.
Ni bora mtu aliyeishi miaka 30 na akaacha alama isiyofutika kuliko mpumbavu aliyeishi miaka 80 ya utegemezi, ya uvivu na isiyo na matokeo.

NIDHAMU KATIKA MATUMIZI YA MUDA.

“…Basi ndugu zangu ANGALIENI JINSI MNAVYOENENDA, si kama wapumbavu bali kama watu wenye HEKIMA huku MKIUKOMBOA WAKATI kwa maana zamani hizi ni za uovu…”
(Waefeso 5:14-16).

Nidhamu katika muda:

•Ishi maisha ya ratiba

Hakikisha una ratiba ya siku, ya wiki na hata ya mwezi mzima.
Maisha yasiyo na ratiba ni maisha yasiyo na uelekeo.
Maisha yasiyo na ratiba yataendeshwa na wenye ratiba kuwafanyia vya kwao.

•Ishi maisha yenye vipaumbele.

Vipaumbele (prioritized life) ni ile hali ya kupangilia mambo yako kwa kuanza na jambo la muhimu zaidi na kumalizia na lenye umuhimu mdogo.
Watu wengi wanaishi maisha ambayo wanafanya vitu bila vipaumbele, matokeo yake wamekuwa washindwa na wengine wamekuwa watu wa wastani badala ya kuwa bora sawa na hazina alizoweka Mungu ndani yao.

•Epuka upotezaji wa muda, komboa wakati.

Fanya mambo ya kesho leo. Fanya mambo ya wiki ijayo wiki hii. Fanya mambo ya mwezi ujao mwezi huu. Fanya mambo ya miezi sita ijayo sasa. Epuka kuwa mzee wa deadline, ukisikia kesho ndio mwisho unakesha usiku mzima, acha hii tabia mbaya ya watu walioshindwa maisha!

3. MADHARA YA KUTUMIA VIBAYA MUDA WA MAISHA YAKO;

i) Utakuwa mtu wa kawaida au wastani, hautakuwa mtu mkuu

ii) Kuna viwango vya maisha utaishia kuviona kwenye ndoto na kwenye tamthilia ila hautaviishi kamwe.

iii) Maisha yako hayatakuwa na thamani wala mvuto. Hautakuwa reference point ya mtu aliyefanikiwa maana mafanikio yatakuwa mbali na mpoteza muda.

iv). Hata siku ya hukumu, kuna uwezekano wa kukwama, maana kila kazi ya mtu itapimwa na ikiteketea umeumia (1Wakorintho 3:13-14)

v) Utakuwa mtu wa mambo ya kawaida, ya wastani na hautakuwa mtu ambaye maisha yako yatakuwa darasa kwa wengine.
Watu wote waliofanikiwa hapa duniani ni TIME CONSCIOUS PEOPLE.

vi) Utakosa FURSA nyingi maishani maana fursa nyingi zina muda maalum, ukichelewa umepishana nazo.

vii) Hautakuwa na ushirika na watu waliofanikiwa bali utakuwa rafiki wa walioshindwa maana watu wote waliofanikiwa hawana muda wa kuchezea, maisha yao yako ndani ya ratiba, hawana dakika kwa ajili ya wapoteza muda.

4. FAIDA ZA KUTUMIA MUDA VIZURI KWA HEKIMA NA NIDHAMU;

i) Utakamilisha kila jambo ndani ya muda, hivyo hutakuwa nyuma au kuwa na viporo.

ii) Utaweza kuipata kila fursa kwa sababu mambo yako yamepangiliwa

iii) Utaepuka upotezaji wa muda

iv) Utajikuta umekuwa karibu na watu sahihi walio serious na maisha

v) Hautakuwa mtu wa kawaida au wa wastani, utakuwa mtu mkuu

vi) Utakuwa kioo cha wengi kwa sababu utafanikiwa sana

vii) Utaepuka watu wasio sahihi kwa sababu wao huambatana na wanaochezea muda

viii) Muda si mrefu jina lako litatamkwa kati ya majina ya watu wakuu

5. MBINU ZA KUTUMIA ILI KUWA NA MATUMIZI MAZURI YA MUDA;

i) Amua kutoka moyoni mwako kwamba kuanzia leo hautachezea wala kupoteza muda.

Ikiwa ni uamuzi wa dhati, akili yako na moyo wako vitakubaliana na utapata hekima na nidhamu ya namna ya kuutumia muda kwa faida.

ii) Punguza muda wa kulala.

Kama una miaka zaidi ya 18, epuka kulala zaidi ya masaa sita kwa siku.
Tumia muda wako nje ya kitanda, kikwepe kitanda na godoro.

iii) Epuka mambo yanayokula muda yasiyojenga yanayoishia kukuburudisha tu bila kujenga roho yako, akili na ufahamu wako.

-Epuka movie, series na tamthilia
-Epuka kuangalia mechi za mpira kwa masaa mengi
-Epuka kutumia simu yako (hasa smartphone) ukiwa kwenye internet kwa zaidi ya masaa 2 kwa siku. Najua wengi mna changamoto ya kulala na simu na kuamka na simu hata kabla ya kuomba na kusoma Neno.

iv) Panga ratiba ya siku (to do list), ya wiki na hata ya mwezi walau.
Maisha bila ratiba ni maisha yasiyo na malengo.
Maisha yasiyo na ratiba ni maisha yanayochezewa.

v) Wekeza muda wako kwenye vitu vinavyojenga na kukuboresha kama vile: Vitabu, Video za mafundisho, semina, makongamano, majarida ya kukuongezea kitu, kuwatembelea na kujifunza kwa watu waliopiga hatua nk!

vi) Kuwa rafiki wa watu strict kwenye muda, ambao wanaishi kwenye ratiba, na wako serious na maisha.
Kumbuka: Ukiambatana na wenye hekima utakuwa na hekima pia (Mithali 13:20).

vii) Hakikisha unanunua notebook ya malengo, mipango, maono na vitu unavyotaka kufanya, viandike, vipitie kila siku, vipe muda wa kuvitimiza, viombee nk!
Hii nayo ni muhimu, itakujenga kuwa focused ili usipoteze muda kwenye vitu visivyo kwenye ndoto zako.

“MANENO YA HEKIMA KUHUSU MUDA NA MWALIMU DICKSON CORNEL KABIGUMILA”

“Maisha ni siku moja moja nyingi alizoishi mtu. Ukitaka kuwa na maisha yenye mguso duniani, anza na kuipangilia siku moja uliyonayo”
(Pst. D.C.Kabigumila)

“Matumizi ya siku yako moja, ni unabii wa maisha yako yote endapo hautabadilisha ratiba yako ya siku na vipaumbele vyako ndani ya siku moja”
(Pst. D.C.Kabigumila)

“Mzee aliyeishi miaka 120 bila matokeo ya kuridhisha ni hasara kwa dunia, mzigo kwa taifa lake na aibu ya ukoo wake. Maisha bila mguso kwa dunia yako ni kama mimba iliyoharibika, na yote haya huanza na ubora katika matumizi ya muda”
(Pst. D.C.Kabigumila)

“Nioneshe mtu aliye makini kwenye kutumia muda wake kujijenga kiroho na kiakili nami nitakuonesha mtu ambaye ana kesho bora mno”
(Pst. D.C.Kabigumila)

“Mtu asiye na nguvu ya kukishinda kitanda na usingizi, ni mtu asiyejua thamani ya muda, na mtu kama huyo umasikini wake utakuja ghafla kama mwivi, na hatakuwa katika orodha ya watu wakuu”
(Pst. D.C.Kabigumila)

MAOMBI
ASUBUHI

1. Muombe Mungu akupe hekima ya kuhesabu siku zako na kuzitumia kwa ubora hapa duniani kuzalisha matokeo makubwa kwa utukufu wa Mungu (Zaburi 90:12).

2. Muombe Mungu akusaidie kuukomboa wakati na kuamka toka uzembe, uvivu na vitu vinavyopora matumizi mazuri ya muda (Waefeso 5:14-16).

MCHANA

3.Muombe Mungu akusaidie kutumia muda wako kwa hekima ili uweze kutimiza kusudi ulilobeba kwa ubora (Mhubiri 3:1).

4. Muombe Mungu akupe ufahamu kwa habari ya nyakati na majira ya maisha yako, ili upate kujua nini cha kutenda katika kila majira ya maisha yako (1Nyakati 12:32).

JIONI
5. Muombe Mungu akusaidie kutumia muda wako kujenga misingi ya vizazi vingi na kuleta mabadiliko (Isaya 58:12).

6. Muombe Mungu akusaidie kutumia muda wako kupanda mbegu njema ambazo uko tayari kuzivuna (Wagalatia 6:6-9).

NB: Niombee mimi Mwl D.C.K nijazwe hekima ya Mungu ya kutumia muda mchache nilionao kwa FAIDA (Isaya 48:17).

Umebarikiwa sana,
Wewe ni wa thamani sana,
Umebeba majibu ya dunia yako!
Tukutane kesho siku ya 10 tuhitimishe pamoja mfungo Huu wa baraka.

Pst. Dickson Cornel Kabigumila,
ABC GLOBAL.
27/02/2019.

Share on facebook
Share on twitter
Share on linkedin
Share on whatsapp
Share on telegram

HEKIMA ZA NDOA 4

“Ndoa ni taasisi ambayo unaungana na mtu mwingine ambaye ANAWEZA KUKUTIA MOTO kwenye KULIFUATA NA KULITIMIZA KUSUDI LA MUNGU… Wawili sahihi kila mmoja anakuwa CHUMA

Read More »

NDOA

“Haiunganishi familia mbili bali inazalisha familia mpya ya tatu… Inayojiendesha, kujitawala, kujiamulia na kujichagulia mambo yake… Familia hii mpya ya tatu inakuwa na kusudi na

Read More »