UKWELI KUHUSU FURSA

 

https://upload.wikimedia.org/wikipedia/commons/b/b1/Book_of_Judges_Chapter_14-3_(Bible_Illustrations_by_Sweet_Media).jpg1. Fursa ziko kwenye vitu vinavyowatisha wengine na kuwaogofya.

-Samson alipata ASALI TAMU kwenye mzoga wa simba.
Hakukuta mzoga wa simba bali ALIMUUA SIMBA KWANZA.
(Waamuzi 14:6-9).
Cha kujifunza: FURSA ZIKO KWENYE KILE AMBACHO WENGI WANAKIOGOPA NA KUKIKIMBIA.
2. Fursa hufanyiwa kazi na watu ambao HUANGALIA UKUBWA WA FAIDA WATAKAYOPATA na kupuuza HATARI ZILIZO KATI YAO NA FAIDA.
-Mbali ya kwamba Daudi alichukizwa na MATUSI YA GOLIATI DHIDI YA MUNGU WAKE lakini bado aliuliza swali: JE ATAFANYIWAJE (ATAPEWA NINI) MTU ATAKAYEMUUA HUYU MFILISTI? Akajibiwa, kuhusu faida: ATAPEWA MIKALI BINTI SAULI, NA FAMILIA YAKE ITAONDOLEWA ISIWE WATUMWA CHINI YA MFALME TENA.
(1Samweli 17:25-27).
Cha kujifunza: Angalia faida iliyomo (zilizomo) ndani ya fursa halafu uone kama inalipa na inafaa kuwekeza nguvu, muda, akili, imani na maisha yako!
3. Fursa haianzi kwa kukuletea WATU WANAOKUUNGA MKONO, Lakini WAKIONA MATOKEO WATAKUPA MKONO WA SHIRIKA.
*Daudi alikatishwa tamaa na ndugu zake (1Samweli 17:28).
*Daudi alikatishwa tamaa na MZOEFU SAULI (Huyu tunaweza kumfananisha na wazoefu kwenye eneo au kitu unataka kufanya), Lakini ALIJENGA HOJA akakubaliwa na Sauli huyohuyo kiasi cha kumpa silaha zake za vita (1Samweli 17:31-38).
Lakini ALIPOMUUA TU GOLIATI; Sauli, ndugu zake, na Jeshi zima la Israeli waliungana naye (1Samweli 17:48-53).
Cha kujifunza: Wape watu muda, hawatakuelewa mwanzoni, lakini mwisho wa siku watakupa mkono wa shirika.
4. Fursa huleta maadui, hii ni kwa sababu fursa zina faida na matokeo ambayo HAYAPINGIKI na yanayo KUHAMISHA KIWANGO KIMOJA KWENDA KINGINE, wanadamu hawapendi watu wawazidi au kuwafikia au kuwakaribia; Jiandae kwa maadui unapoifuatilia fursa!
-Ndugu wa Daudi walimchukia.
-Mfalme Sauli alitaka kumuua mara nyingi.
-Walimu wa sheria na makuhani walihatarisha maisha ya Yesu mara nyingi.
-Yakobo alikuwa adui mkubwa wa Esau sababu ya fursa ya baraka aliyoinunua kwake kupitia mlo mmoja wa dengu.
Cha kujifunza: Mungu aliyekupa fursa atakuokoa na mikono ya adui zako (Warumi 8:31).
5. Fursa inabeba baraka zaidi ya mahitaji yako, inagusa watu wa nyumba yako, taifa na hata dunia yako.
-Asali aliyoipata Samson hata familia yake walikula, haikuishia kwake (Waamuzi 14:6-9).
-Mojawapo ya faida za kumshinda Goliati alizopewa Daudi ilikuwa: FAMILIA YAKO HAITAKUWA TENA WATUMWA WA MFALME (1Samweli 17:25-27).
-Yusufu alipokwenda Misri na kupata nafasi; ALIILETA FAMILIA YAKE MISRI, AKAITUNZA MPAKA ALIPOKUFA.
Cha kujifunza: Chochote ambacho kinaishia kwako tu, SI FURSA, achana nacho.
6. Watu wanaoweza kufaidi FURSA ambazo Mungu anazileta mbele zao ni watu WENYE UHODARI NA MIOYO YA USHUJAA PEKE YAO.
– Musa alipokufa, ilitokea Fursa kwa Joshua ya kuongoza taifa la Israeli kuelekea Kanani.
Mungu alimwambia “UWE HODARI NA USHUJAA MWINGI KWA MAANA WEWE NDIYE UTAKAYEWARITHISHA NCHI WATU HAWA” (Yoshua 1:6).
Mungu alikuwa anamuambia: “Ndani ya fursa hii moja kuna maisha ya mamia elfu hawa wote, usijihurumie, usikubali kukata tamaa, KUJIHURUMIA AU KUKATA TAMAA KWAKO KUTAHARIBU DESTINY ZA WATU WOTE HAWA”
Kitakachokupa ujasiri wa kuendelea KUKAMATA FURSA ni kujua kuwa WATU WENGI SANA WAMEFUNGWA KWENYE FURSA YAKO!
Umewahi kujiuliza Mzee Kulola angeikatia tamaa EAGT? CAG, FGBF na wengine wengi wangetokea wapi? (Japo Mungu huenda angeleta wokovu kwa namna nyingine)!
-Daudi alikuwa hodari na ushujaa mwingi ulijaa ndani yake: HAKUONA CV KUBWA YA GOLIATI kuwa kitu akiangalia UHURU WA WENGI kama ataibuka kidedea.
-Yesu hakuangalia MASLAHI BINAFSI (kikombe hiki kiniepuke), bali ALIUANGALIA ULIMWENGU AKAUPENDA NA KUKUBALI KUWA SADAKA KWA AJILI YAKE.
Cha kujifunza: Ukitaka kuifuata fursa na kupata matokeo, jitoe, beba picha kubwa ya utakaowagusa, angalia utukufu utakaokujia ukipenya na puuza hali ngumu ulizonazo sasa.
7. Fursa haziwanufaishi watu wengi wenye vigezo na viwango.
Mara nyingi Mungu huleta fursa kwa watu ambao hawakutarajiwa, waliodharauliwa, wasio na elimu kubwa au wasio na elimu kabisa, wasio hodari na wasio na wa kuwashika mikono.
-Petro hakuwa na elimu (Matendo 4:13).
-Musa alikuwa na kigugumizi na alikuwa muuaji (Kutoka 2:11-14, Kutoka 4:10-12).
-Yusufu alikuwa mtumwa nyumbani kwa Potifa, mfungwa gerezani (Mwanzo 39 yote).
-Rahabu alikuwa kahaba (Yoshua 2:1, Yoshua 6:17,23-25, Waebrania 11:31).
Cha kujifunza: Wewe hivyo ulivyo unafaa kupewa fursa kubwa na Mungu, kaa naye vizuri. Kuna siku tutakutana ukiwa mtu mwingine.
8. Fursa hujificha katika vitu vidogo na vya kawaida mara nyingi.
-Rahabu alipokea wageni ambao hakujua walibeba fursa ya kuponya maisha yake na ndugu zake wote.
Kwa “kupokea wageni” ikawa ni fursa kubwa iliyogeuza jumla maisha yake.
(Yoshua 2:1-3, Yoshua 6:17-25).
-Yusufu alisimuliwa ndoto na “wafungwa wenzie” wawili, akazitafsiri. Na kupitia tukio hilo la ukarimu, kusikiliza na kujali wengine, akapata mlango wa kuingia Ikulu kwa Farao, japo ilichukua miaka miwili tangu atafsiri ndoto ile gerezani.
(Mwanzo 40 yote, Mwanzo 41:1-16).
9. Mungu akikupa fursa, MKONO WAKE UNAAMBATANA NA WEWE kukusaidia kikubwa USIENDE DHAMBINI NA KUUPOTEZA UWEPO WAKE.
Siri kubwa ya waliopata fursa na kuzitumia kwenye Biblia, ni KUTOCHEZA NA UHUSIANO WAO NA MUNGU. Hawakuruhusu yeyote au chochote kiingilie NAFASI YA MUNGU, MUDA WAO NA MUNGU NA UHUSIANO WAO NA MUNGU.
-Yusufu
“BWANA akawa pamoja na Yusufu naye akastawi” (Mwanzo 39:2).
Siri ya KUSTAWI KWA YUSUFU ilikuwa “BWANA kuwa naye na kuendelea kuwa naye”
Alijua akimpoteza BWANA kapoteza na ustawi.
Hata mke wa Potifa alipotaka kuzini naye alimjibu “NITENDEJE UBAYA HUU MKUBWA NIMKOSE MUNGU (NIPOTEZE UWEPO WA MUNGU)?”
(Mwanzo 39:9).
Kumkosa Mungu ni kupoteza ustawi katika fursa!
-Yesu
Nikodemo alikuwa mwalimu mashuhuri wa torati katika Israeli, alikaa chini akaisoma na kuipima huduma ya Yesu, na akaja na jibu moja muhimu sana; “Mwalimu, UMETOKA KWA MUNGU; Kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi ufanyazo wewe, isipokuwa MUNGU YU PAMOJA NAYE”
(Yohana 3:2).
Petro anasema kitu kilekile kuhusu Yesu na huduma yake kwenye Matendo 10:38.
“…KWA KUWA MUNGU ALIKUWA PAMOJA NAYE”
Wengine:
-Musa alikuwa na ishara (fimbo, mkono kuwa na ukoma), lakini ALITUNZA MNO UWEPO WA MUNGU.
-Daudi alipakwa mafuta na Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, lakini pia ALIUTUNZA MNO UHUSIANO WAKE NA MUNGU, hata alipojikwaa HAKUMKIMBIA MUNGU BALI ALIMKIMBILIA MUNGU.
Cha kujifunza: Watu wa fursa ni watu wa kuheshimu nafasi ya Mungu kwao, muda wao na Mungu na hawaruhusu chochote kuharibu mahusiano yao na Mungu.
Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila
Mawasiliano:
www.yesunibwana.org
kabigumilacornel.dick@gmail.com
Simu: +255- 655/753- 466 675
Kwa mialiko ya kihuduma, maoni na ushauri.

Share on facebook
Share on twitter
Share on linkedin
Share on whatsapp
Share on telegram

KWA WAOAJI TU

“Ni Hekima Ya Mungu Kumpa Mwanadamu MALIGHAFI [Raw Materials] Ili Yeye [Mwanadamu] Afanye Sehemu Yake KUZIFANYA KUWA BIDHAA HALISI [Products]… Mungu Anakupa MTI Na Ni

Read More »

usioe kwa sababu

“Usioe kwa sababu unawaka tamaa, hivyo unaoa ili usiendelee kutenda dhambi nje. Dawa ya tamaa si kuoa. Dawa ya tamaa ni kukubali kuwa tamaa inakutesa,

Read More »

HEKIMA ZA NDOA 3

  “Kusudi la ndoa ni kujenga TIMU YA WANAOSADIANA NA KUINUANA. Wawili ni bora kuliko mmoja, MAANA MMOJA AKIANGUKA, MWENZIE ATAMUINUA. Ndoa sahihi ni muunganiko

Read More »