MFUNGO WA SIKU 10,MASAA 12 -APRIL [SIKU YA 7]

KANUNI YA UKUAJI (THE PRINCIPLE OF GROWTH).

Utangulizi

Maisha ni hatua, na hatua mojawapo ya muhimu mno na ya lazima kwenye maisha ni ukuaji!

Usipokua maana yake umedumaa.

Kudumaa ni kukosa ukuaji chanya, ni kushindwa kupiga hatua kwenda mbele au kwenda juu kwenye kilele cha ubora na mafanikio!

Mtu asiyekua ana kasoro, Mungu hakuumba mtu au kitu chochote kibaki katika hali moja milele.

Kitu kinapita kwenye hatua kadhaa kama vile; kuzaliwa, kukua, kukomaa, kutoa matunda na kufa.

Lakini katika yote hapo juu, linaloendelea wakati wote ni kukua pekee.

Kuzaliwa hutokea mara moja, kukomaa hutokea baada ya muda fulani, matunda huja/ hupatikana kwa msimu au misimu kadhaa, kufa hutokea mara moja,lakini ukuaji ni kitu pekee endelevu!

Maandiko yanasema;

“Sisi ni miti ya haki tuliopandwa na Mungu ili kupitia sisi Mungu atukuzwe”

(Isaya 61:3).

Na kama ilivyo miti yote, inapaswa ikue, ifike mahali pa kutoa matunda au mbao/zao la kuvunwa.

Mti usiokua na kuleta matunda au zao, huo ni mti ambao haukutimiza kusudi la uwepo wake.

MAHITAJI MUHIMU ILI KUTIMIZA KANUNI YA UKUAJI;

1. MIZIZI

Ukikosa mizizi, utaonekana kwa kitambo, lakini baada ya muda utakauka/ hautafikia lengo la kuzaa matunda (Luka 8:13).

Mmea wowote ambao hauna mizizi, hauna uwezo wa kuvuta maji na chakula toka ardhini, baada ya muda utakonda, utasinyaa na kukauka.

Vivyo hivyo, mtu ambaye halipi gharama kujijenga kwenye kanuni sahihi za Ufalme wa Mungu katika Neno na kanuni sahihi zinazotawala maisha, mtu huyu hata kama ana uthubutu na nia nzuri, hawezi kukua!

MIZIZI INAWAKILISHA MSINGI MZURI KATIKA MAENEO YOTE UNAOKUPA KUKUA KWA USAHIHI NA UBORA.

2. UDONGO

Mmea/mche wowote ili ukue na kuleta matokeo hauhitaji mizizi tu.

Mizizi ikiwepo lakini bila UDONGO mti hauwezi kukua.

Udongo unatoa mambo kadhaa kwa mmea;

•Mahali pa kusimamia

Udongo ni mahali pa kusimamia mmea (base/ standard).

Mahali shina la mmea linaposimama ili kutoa matokeo tarajiwa.

•Mahali pa kujengwa na kukulia hata majira ya kuleta matunda au zao.

•Mahali pa kuchukua maji na chakula ambavyo ndivyo huchochea ukuaji.

Kwa maana hizo tatu, udongo ni mzazi wa kiroho ambaye anamsaidia mtu kutimiza kusudi la kuumbwa kwake.

Mtu asiye na baba wa kiroho anakosa mambo haya matatu tajwa hapo juu;

-Msingi (base/standard)

-Kujengwa na kukuzwa

-Chakula sahihi na nguvu ya Kiungu ya kumkuza kuwa mtu kati ya watu.

Nakushauri, uwe mnyenyekevu, ukubali kuwa chini ya baba wa kiroho aliye na mambo haya makuu matatu, ili akusaidie kukua na kuwa mtu mwenye matunda kwenye maisha.

Sasa usinielewe vibaya, ukadhani nasema hili ili kujipigia upatu uwe mwanangu wa kiroho, la hasha! Kila mmea una aina ya udongo sahihi wa kuukuza na kuufanya utoe matunda, siwezi kuwa baba sahihi wa kila mtu.

Namshukuru Mungu, mimi ninaye baba wa kiroho, nabii wa Mungu, Emmanuel Makandiwa wa huduma ya UFIC kule Zimbabwe.

3. NGUVU YA KUKUA

Ili mmea wowote ukue na kufikia mahali pa kutoa matunda au mbao (zao) lazima uwe na nguvu ya kukua.

Nguvu hii inahusisha mambo kadhaa;

•Utayari wa mmea kukua.

Mmea usiporuhusu mizizi itokeze, usiposhusha mizizi ardhini, usiponyonya maji na chumvi (kujilisha), hata ungetaka kuusaidia kivipi, hauwezi kukua!

•Maji na chakula toka kwenye udongo.

Maji na chakula hutoka ardhini/ udongoni.

Bila mti kujiungamanisha na udongo, hautapata kilichoko udongoni, utakosa maji na chakula ambavyo ni lazima mno kwa ajili ya ukuaji.

Ndivyo pia ilivyo kwa mtu ambaye hana baba wa uhakika aliyebeba maji (upako) na chakula (Neno sahihi) la kumkuza, hawezi kuwa mtu mkuu aliyekusudiwa na Mungu.

•Nuru/Mwanga

Mmea kuwa na utayari kukua, kuungana na udongo sahihi wenye maji na chakula, si kigezo pekee cha ukuaji.

Mmea wowote ili ukue unahitaji mno nuru.

Maandiko yanasema Mungu ni nuru (1Yohana 1:5).

Ili tukue na kuwa na matunda ni lazima tuwe na ushirika na Nuru/Mungu (1Yohana 1:6-7).

Pasipokuwa na ushirika binafsi wa kina na Mungu (Nuru) hata tuwe na mababa wa kiroho (udongo) wazuri mno, HAKUNA UKUAJI.

BABA YEYOTE WA KIROHO ANAJUA YA KUWA HACHUKUI NAFASI YA MUNGU MAISHANI MWAKO.

ANAJUA UNAPASWA KUWA NA UHUSIANO NA USHIRIKA BINAFSI NA MUNGU NA ANAKUSAIDIA KUMJUA MUNGU WA KWELI NA WA PEKEE NA YESU ALIYEMTUMA (Yohana 17:3).

Udongo ni wa muhimu, lakini unajua ULAZIMA NA UMUHIMU MKUBWA MNO WA NURU KATIKA UKUAJI WA MMEA.

Mjue sana Mungu ili uwe na amani, ndivyo mema yatakapokujia (Ayubu 22:21).

Bali watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari na kutenda mambo makuu (Danieli 11:32).

Kwa msaada wa Mungu, tutatenda mambo makuu, maana Yeye (Mungu) atawaseta adui zetu (Zaburi 60:12).

Mmea unaweza kuchukua maji na chumvi toka kwenye udongo, lakini ili uweze kujitengenezea chakula unahitaji NURU YA JUA ILI KUKAMILISHA UTENGENEZAJI CHAKULA, HAKUNA NURU, HAKUNA CHAKULA KWA MMEA.

Hii ina maana baba wa kiroho anaweza kupanda vitu vingi kwako, akamwagilia kwa maombi mengi na machozi, lakini MUNGU PEKEE NDIYE AKUZAYE NA KUINUA (1Wakorintho 3:6-7).

Nuru pia inawakilisha ufahamu, akili, ujuzi na ufunuo sahihi wa kukusaidia kuwa mtu kati ya watu.

Na maandiko yanasema YESU KRISTO PEKEE NDIYE NURU HALISI IWATIAYO NURU WATU WOTE (Yohana 1:6-12).

Yeye amwaminiye yeye hata kwenda gizani kamwe BALI ATAKUWA NA NURU YA UZIMA (Yohana 8:12).

Kama unataka kustawi na kuchanua kwenye maisha haya na kisha uwe na uzima wa milele, MPOKEE YESU ALIYE NURU ILI AKUTIE NURU.

OMBA SALA HII YA TOBA KWA IMANI:

Mpendwa Bwana Yesu,

Mimi ni mwenye dhambi,

Naziungama dhambi zangu zote leo nikimaanisha kuziacha,

Ninaamini ulikufa msalabani kwa ajili yangu ili niokolewe na siku ya tatu Mungu Baba alikufufua toka katika wafu,

Toka leo ninakufungulia mlango wa moyo wangu,

Kwa imani nimeokoka katika jina la Yesu,

AMEN.

Ikiwa umefanya uamuzi huu, umejiunga na Nuru halisi yaani Kristo Yesu na Mungu wa Kweli na wa pekee aliyemtuma!

HONGERA KWA KUOKOKA.

•Hali ya hewa

Hali ya hewa ni kigezo pia katika ukuaji wa mmea.

Kuna mimea inastawi maeneo ya joto na mingine inastawi zaidi kwenye ukanda wa baridi.

Hali ya hewa sahihi inayosaidia ukuaji wa mtu ni UWEPO WA ROHO MTAKATIFU MAISHANI MWAKE.

Huyu Roho wa Mungu pekee, ndiye aletaye hali (environment/ atmosphere) ambayo inapelekea ukuaji sahihi wa mtu hata kufika mahali pa kuzaa matunda na kuwa baraka kwa dunia yake.

Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wetu alijua hili, ndio maana aliwaagiza Mitume wasitoke Yerusalemu MPAKA WAVIKWE NGUVU.

Halafu baada ya hayo WATAKUWA MASHAHIDI WAKE (WATAKUA NA KUWA NA MATOKEO) KWENYE MAISHA YAO (Matendo 1:8).

Bila Roho Mtakatifu maishani mwako, kuna kitu unakikosa maishani mwako kwakuwa; WALE WOTE WAONGOZWAO NA ROHO WA MUNGU, HAO NDIO WANA WA MUNGU (Warumi 8:14)!

Baada ya kuokoka, na kuwa na ushirika binafsi na Mungu, na kuwa na Mzazi sahihi wa kiroho, lakini HAKIKISHA UNAMFAHAMU KIBINAFSI HUYU ROHO MTAKATIFU (Tafuta kwa bidii masomo, vitabu, video kuhusu Roho Mtakatifu, wafuatilie watumishi hawa wa Mungu wana uelewa mzuri kuhusu Roho Mtakatifu: Benny Hinn, Pastor Chris, David Diga Hernandez, Pastor Vlad)

Ukizingatia haya, KUENDELEA KWAKO (KUKUA KWAKO) KUTAKUWA DHAHIRI MBELE ZA WATU WOTE!!

MAOMBI

1. Muombe Mungu akusaidie kuwa na shauku isiyoisha ya kukua katika maeneo yote ya maisha (1Wakorintho 13:11)

2. Muombe Mungu akusaidie kupandwa katika udongo mzuri (mzazi sahihi wa kiroho) kwa wale ambao hawana wazazi wa kiroho.

Kama una baba wa kiroho tayari, Muombe Mungu akusaidia kutii na kunyenyekea kwa baba/ mzazi huyo ili uweze kupokea toka kwake ya kwako aliyobeba!

3. Muombe Roho Mtakatifu akusaidie kuwa na ushirika wa kina binafsi wako na Mungu aliye hai katika Kristo Yesu

4. Tamani na kuwa na shauku isiyoisha ya kuwa na ushirika na Roho Mtakatifu; Mwambie Roho Mtakatifu kiu na shauku yako kwake (Zaburi 63:1-3).

5. Muombe Mungu akupe kukua kila siku ili uweze kupata haki na urithi wako ndani yake, ambao unahitaji ukue ili upewe (Wagalatia 4:1-3)

Umebarikiwa mno,

Wewe ni mtu wa muhimu kwa dunia yako,

Amua kuwa suluhu ya maisha ya wengi na furaha ya vizazi vingi!

Tukutane kesho siku ya nane ya mfungo huu.

Pst. Dickson Cornel Kabigumila

Mchungaji kiongozi,

Assembly Of Believers Church (ABC),

28/04/2019.

Usiache kutembelea tovuti yangu ya mafundisho ya:

www.yesunibwana.co.tz

NB: ENDELEA KUANDAA SADAKA YAKO NZURI YA KUAMBATANISHA NA MFUNGO HUU, AMBAYO UTAITOA SIKU YA KUHITIMISHA MFUNGO YAANI TAREHE 01/05/2019.

Mafundisho
yesunibwana

SEX BEFORE MARRIAGE

#TENDO LA NDOA KABLA YA #NDOA Luka 16:10 [10]Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo

Read More »