Shuhuda(Testmonies)

Mimi niliamua kumleta mke wangu hapa ili aombewe tu aache pombe na tumbaku na mguu wake ambao umekuwa ukimsumbua na tangu tuoane sasa tumezaa watoto 11 na saba wako hai, lakini mke wangu amekuwa akinywa pombe na tumbaku hadi anarudi saa tisa za usiku! Na kwa vile alikuwa akiona aibu, kila akifika hapa anajificha vichakani, leo nimeamua kumleta kwa nguvu.

Alikuwa kila akifika, anasimama mbali zaidi vichakani ndipo nilipoamua kumvuta na kumleta hapa pamoja na kuwa alikuwa akipiga kelele! Sisi katika dini yetu, hatuna utaratibu huu wa kuombea na kuwatoa watu mapepo. Tumehangaika sana kwa waganga, haachi pombe wala tumbaku na huo mguu ambao sasa nashangaa anarukaruka akiimba, sijui nguvu hizo katoa wapi?

Hayo yamesemwa na Mzee Edward Mtatiro (69) mkazi wa Kitongoji cha Ngano Kijijini Msake, Kata ya Minyughe Tarafa ya Ihanja Wilayani Singida Vijijini ambaye alifika mkutanoni siku ya jumapili jioni saa 11 wakati mahubiri ya nje yakielekea mwisho wake akiwa amelewa chakari na kuanza kusemasema hovyo maneno yasiyo eleweka na kuwafanya wasikilizaji wa mkutano huo wamshangae na wengine wakicheka

Mchungaji Benard Jomalema aliamua kuwaomba wenyeji waliotaka kumtoa wamwache tu na wamwache aendelee kwa vile alikaa katikati kabisa ya watu na kuruhusu Mch Jonathan aendelee tu na mahubiri.

Mahubiri yalipoisha, wakatokea watu waliopagawa mapepo na wengine walioomba kuombewa tu kibandani. Baba huyo alitokea tena ghafla akimburuta mkewe wakiwa wote wamelewa na kumwingiza katika banda la maombezi. Walipoingia wakapewa kiti, na kueleza amaechoka na shida za kila siku za mkewe! Hivyo anaomba aombewe.

Mchungaji Jonathan akamkubalia, na mama huyo alipoulizwa kama yuko tayari kuombewa akakubali huku akitamka kwa kumumunya mumunya maneno. Mchungaji akamwambia, haya nishike mikono, alipoweka tu mikono yake juu ya mikono ya mchungaji, ikawa kama mtu aliyerushwa na umeme huku akielekea kumparamia mchungaji aliyemkwepa na kumshika asiangukie uso, ukawa kama ni mchezo wa sinema tu.

Ndipo mapepo yalipoanza kupiga kelele kama aliyevamiwa nyumbani kwake usiku wa manane na anaomba msaada! Watu waliokuwa nje wanaanza kuondoka ondoka wakazingira kibanda cha maombezi kutaka kujua kulikoni. Mumewe huku akiwa amelewa, alianza kupiga kelele, mtoe huyo pepo mtoe!

Maombi yalipoendelea, Mzee Edward akawa amechoka akatoka zake nje na kuendelea kusubiri. Hata hivyo subira yake haikuendelea bali alirudi ndani na kukuta mkewe bado anagalagala chini na kutamka maneno yasiyoeleweka huku akiendelea kuombewa.

Mzee Edward ambaye kila wakati alikuwa akiuliza, lakini ni kwa nini ninyi mnamfundisha kusema Kiarabu, alichoka na kuanza kupiga kelele za kuwaomba wamuache aende nyumbani. Watumishi waliendelea na maombi na kumwombea “rehema na kweli” ili Mungu amsamehe na kumwokoa.

Bila ajizi Mama huyo aliyezinduka na kuanza kushangaa kama mtu aliyepotea akiwa na akili timamu na kuuliza hapa niko wapi na nimefikaje! Lakini hakuna aliyemjibu bali mumewe alimchukua taratibu wakaishia nyumbani kwao. Mama huyo sasa amepona kila kitu na mumewe ameshuhudia siku ya mwisho ya semina hajamwona mkewe akitumia tumbaku, akichechemea wala kunywa pombe bali amekuwa tu kama aliyenyeshewa mvua lakini mwenye furaha. Kwa sasa mama huyo amebatizwa akiitwa Elizabeth na bintiye mwingine mwenyeumri wa miaka 17.

chanzo…….HIKI HAPA

7 thoughts on “Shuhuda(Testmonies)”

  1. Hakika Mungu Hana upendeleo. Wokovu na uponyaji wake ni wa bure kwa watu wote. Asante mchungaji kwa kupeleka injili hata kwa wanyaturu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *