SIKU YA NNE, FEBRUARI 22/2019
KANUNI YA NGUVU (THE PRINCIPLE OF POWER).
Utangulizi
Maisha yanatawaliwa na kanuni ya nguvu.
Wenye nguvu wanastawi kwenye maisha, walio dhaifu wanatawaliwa.
•Wenye bidii hutawala bali wavivu hutozwa kodi (Mithali 12:24).
Hii ni kwa sababu bidii ni nguvu kubwa kuliko uvivu.
•Matajiri huwatawala masikini na wakopaji hutawaliwa na wakopeshaji (Mithali 22:7).
Ni kwa sababu pesa na mali ni nguvu bali umasikini na ufukara ni unyonge.
•Wenye akili hupewa nafasi za kiuongozi na wajinga hutawaliwa (1Samweli 18:5, Mwanzo 41:39-40).
Hii ni kwa sababu akili ni nguvu na ujinga ni mzigo.
•Nuru hulitawala giza na ni njema kuliko giza (Mhubiri 2:13).
Ni kwa sababu nuru ni nguvu na giza ni udhaifu!
•Hekima ni bora na muhimu kuliko upumbavu (Mhubiri 2:13).
Ni kwa sababu hekima ni nguvu kubwa kuliko upumbavu.
•Wingi wa watu sahihi maishani ni bora kuliko uchache wa watu sahihi maishani (Mithali 14:28).
Hii ni kwa sababu wingi ni nguvu na uchache ni udhaifu.
Kwa mifano hii, unaona kabisa ya kuwa ulimwengu unatawaliwa na kanuni ya nguvu.
Wenye nguvu za namna mbali mbali ndio huwatawala wanyonge na wadhaifu!
UKWELI KUHUSU KANUNI YA NGUVU;
1. Huwezi kufanya lolote bila nguvu (Wafilipi 4:13).
2. Huwezi kuzaa matunda yoyote maishani pasipo nguvu (Isaya 37:3).
3. Huwezi kuwa tajiri au kuupata utajiri bila nguvu (Kumbukumbu 8:18).
4. Huwezi kutiisha mamlaka nyingine bila nguvu kubwa kuliko yao (Mathayo 12:29).
5. Huwezi kujulikana au kuenea bila nguvu (Luka 4:14).
6. Huwezi kuwa shahidi wa Yesu unayeeleweka bila nguvu (Matendo 1:8).
7. Huwezi kujenga imani sahihi kwa watu kuhusu Mungu bila udhihirisho wa wazi wazi wa nguvu za Mungu (1Wakorintho 2:4-5).
8. Huwezi kutiisha mamlaka na nguvu za kuzimu bila kuwa na nguvu kubwa ya Mungu (Luka 10:19, Luka 9:1-2).
9. Huwezi kuvipata na kuvifurahia vitu vilivyo kwenye Ufalme wa Mungu bila nguvu (Mathayo 11:12).
10. Hekima ni nguvu kubwa inayotawala nguvu nyingine na inayoleta nguvu nyingine (Mithali 4:7, Mithali 24:3-5, 1Wafalme 3:1-15).
11. Huwezi kwenda juu na kupiga hatua za mafanikio/kupanda juu bila nguvu kubwa (Isaya 40:28-31).
MAOMBI
ASUBUHI
1. Muombe Mungu awe sehemu ya maisha yako (fungu lako), ili akuwezeshe kutenda yote kwa nguvu zake (Maombolezo 3:24, Wafilipi 4:13).
2. Mtake BWANA na nguvu zake, na uwe na kiu na shauku ya kuutafuta uso wake kila siku (Zaburi 105:4, Zaburi 63:1-3).
MCHANA
3. Muombe Roho Mtakatifu akufanye kuwa hodari katika BWANA na katika uweza wa nguvu zake (Waefeso 6:10).
4. Muombe Roho Mtakatifu kila siku ayajaze maisha yako, ili uwe na nguvu za kusababisha matokeo kwenye eneo lako la kusudi na wito uliobeba kwenye maisha (Matendo 1:8).
JIONI
5. Omba Mungu akupe nguvu za kuupata utajiri na kustawi kiuchumi na kimaisha kama mwana wa Mungu kadri Roho yako ifanikiwavyo (Kumbukumbu 8:18, 3Yohana 1:2).
6. Muombe Mungu akupe UWEZO wa kuzaa kila wazo, mpango, ndoto, maono, vipawa ulivyobeba, usiishie kuota ndoto bila vitu kutimia maishani mwako (Isaya 37:3, Isaya 66:7-9, Wafilipi 1:6-7)!
NB: Niombee mimi Mwl D.C.K Bwana azidi kunihifadhi, na kunijaza nguvu zake za UTAKATIFU, uadilifu na kusimamia Kweli yake bila kuipindisha (Matendo 1:8, Matendo 4:29-31).
Umebarikiwa mno,
Wewe ni jibu la maisha ya wengi,
Dunia inasubiri majibu toka kwako.
Tukutane kesho siku ya tano,
Pst. Dickson Cornel Kabigumila,
Mchungaji kiongozi,
ABC GLOBAL.
22/02/2019